KING CHAVALA: Msomi anayetaka kuleta mabadiliko fani ya uchekeshaji
“IMEKUWA kawaida kwa wasanii wa vichekesho kupenda ama kuwa na hulka ya kuchekesha huku wakiwa katika hali ya uchafu na kutokuwa na elimu ya kutosha, hivyo mimi licha ya kuwa msomi wa chuo kikuu nimeamua kuwa mchekeshaji.”
Hayo ni maneno ya msanii, Fred Chavala ‘King Chavala’, ambaye anasema ili kubadili hali hiyo ameamua kuleta mageuzi ya tasnia ya uchekeshaji kwa kuleta ‘Standard Comedy’ nchini.
Chavala ambaye ni mhitimu wa fani ya Usimamizi wa Biashara na Utawala, amejiajiri katika kazi ya uchekeshaji, ambayo huifanya katika majukwaa na matamasha mbalimbali nchini.
“Pia ninafanya kazi kama mshauri wa kujitegemea wa Usimamizi wa Biashara na Utawala katika sehemu mbalimbali na hata kwa mtu mmoja mmoja,” anasema.
Katika harakati zake za kuingia kwenye usanii, Chavala anabainisha kwamba, binafsi ndiye alijigundua kwamba ana kipaji, hivyo akaweka nguvu zaidi ili aweze kukiendeleza na kudai amefanikiwa katika hilo.
“Baada ya kugundua kwamba nina kipaji na kinalipa, nikaamua kujikita huko zaidi, hapa simaanishi kwamba kuna fedha nyingi sana la hasha, bali namaanisha kwamba, huku kuna amani, hakuna vurugu na nimeridhika kuwa huko,” anasema Chavala.
Akizungumzia kuhusu kazi, anasema kwamba anafanya kazi hata kwa mwezi mmoja bila ya kupata fedha, lakini kwa kuwa ana amani moyoni, huwa anaridhika na kazi zinakwenda.
Akifafanua kilichosababisha asipende kuajiriwa, anasema kwamba, kazi ya kutumwa ni sawa na utumwa, hivyo baada ya kujitambua ana vipaji na hasa katika uchekeshaji, akaamua kufanya kazi hiyo kwa kujiajiri mwenyewe mwaka 2001.
Hata hivyo, katika utekelezaji wa majukumu yake, anasema anakumbana na changamoto mbalimbali, lakini kubwa linalomkabili ni namna watu wanavyochukulia sanaa ya uchekeshaji kama ni kuvaa nguo chafu au kuvaa malapa, yaani kwa ujumla kutokuwa nadhifu.
“Kutokana na hali hiyo, nikawa na wazo moja la kutaka kubadili mtazamo huo na nilipomaliza elimu yangu ya chuo kikuu nikaamua kuwa mchekeshaji msomi, ninayeijua kazi yangu kwa kuifanya kitaalamu zaidi,” anasema.
Chavala anawataja baadhi ya watu waliomvutia kisanii kuwa ni pamoja na Chrisrock wa nchini Marekani, Mr. Bean wa Uingereza, Charlie Chaplin na Nouh Travor wa Afrika Kusini.
Anasema yeye huwa anawaangalia sana wachekeshaji hao, huku akitamani siku moja Watanzania weweze kumuelewa kila anachokifanya.
Malengo yake ya sasa msanii huyu anasema ni kutoa elimu kwa kuwafundisha baadhi ya watu, ili waweze kufanya ‘Standard Comedy’ kwa mafanikio makubwa.
Ndani ya mwaka huu, anasema amejiwekea malengo ya kufundisha watu wasiopungua 200 katika mikoa mitano nchini, ambapo atafanya ziara maalumu.
Anasema, ziara hiyo ambayo ataanza kuifanya kati ya Julai hadi Desemba mwaka huu, atazuru mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Arusha, Tanga, Dodoma na Mbeya.
Chavala anaongeza kuwa kazi hiyo anafanya kwa kujitolea zaidi, kwani amejaribu kuomba udhamini lakini hadi sasa anapoteza matumaini ya kupata na kusisitiza kwamba, yeye atatimiza njozi hiyo ya kutoa elimu hata kama atakosa udhamini.
Wito wake kwa wazazi, Chavala ametaka kuwapa nafasi watoto wao ambao wanaonesha wana kipaji fulani na kudai kwamba hata yeye awali alipata wakati mgumu sana kuelewana na wazazi wake, kwani hawakumuunga mkono katika chaguo lake la kazi anayoifanya, tofauti na alichokisomea shuleni na chuoni.
Kwa upande wa vijana, amewataka kupenda mambo yenye asili ya Kitanzania, badala ya kuendekeza vitu vya nje na kuongeza kwamba, hii ndiyo sababu kubwa iliyomfanya kutaka kutoa elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa kuipenda sanaa, kwani kupitia huko wanaweza kujiajiri na kupambana na changamoto mbalimbali katika maisha.
King Chavala anasema katika matarajio yake anatamani siku moja awe balozi wa wachekeshaji, ambaye atapeperusha vema bendera ya nchi ikiwamo kufanya kazi Hollywood.
Historia ya Chavala inaonesha elimu yake ya msingi aliipata katika Shule ya Mwenge, Dar es Salaam kabla ya kujiunga na kidato cha kwanza hadi cha nne katika Sekondari ya Viwawa mkoani Mbeya na kidato cha tano na sita katika Shule ya Ufundi Tanga.
Pamoja na kuwa mchekeshaji, pia tayari ameandika vitabu viwili vyenye maudhui ya kuleta uhamasishaji miongoni mwa wasomi, ambavyo ni ‘No More School For You’ na ‘Can a Black Balloon Fly’.
Mbali ya kuwa mchekeshaji, King Chavala ni mwimbaji wa nyimbo za muziki wa Injili na mshereheshaji (MC), katika shughuli mbalimbali kama harusi, matamasha ya kidini, mikutano, semina, misiba na matukio mbalimbali.
SOURCE;http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=45997